Katika maisha
mawazo ni kitu cha kawaida kwa mwanadamu, lakini hata hivyo matumizi ya
akili lazima yawekewe mipaka na isiwe ni kitu cha kawaida ubongo
kuruhusiwa kwenda mwendo mkali kulingana na uwezo wake.
Waundaji wa
mashine, kwa mfano, wakati wanatengeneza injini waliweka mwendo kasi wa
kiwango cha juu, hata hivyo huonya kuwa si kila wakati mwendesha chombo
cha moto anaruhusiwa kutumia ‘spidi’ zote zilizomo ndani ya mashine
yake.
Hali hiyo
ndiyo inayojitokeza katika uwezo wa ubongo katika kufikiri na kupata
majibu ya kina ya nini kilichopo na kitakachotokea. Ni ukweli ulio wazi
kwamba ubongo ni mashine kubwa yenye uwezo wa ajabu usioelezeka.
Watu wengi waliofanikiwa na wanaotaka kufanikiwa ni wale ambao wanajua namna ya kuutumia ubongo katika kupanga maisha yao.
Kila unachokiona ni zao la ubongo kwani mawazo ndiyo mwanzo wa kila
kitu kilichopo duniani. Binafsi naamini hata Mungu aliweza kabla ya
kuumba ulimwengu.
Lakini pamoja
na umuhimu wa mwanadamu kutumia akili yake kupata majibu ya hisia,
maono, mazingira na vitu anavyokutana navyo maishani, kuna wakati
umuhimu huo hukosa maana na maonyo ya kuwa na udhibiti kasi ya fikra
yanachukua nafasi.
Haijalishi
mhusika ana uwezo wa kiasi gani ndani ya akili yake! Kumbuka pia onyo la
dereva kutumia mwendo kasi kila anapowasha gari lake, halafu linganisha
na akili yako au ya mwanadamu unayemtazama utagundua kuwa kithibiti
mwendo kinahitajika hata katika mawazo.
Hebu
chukua jukumu la kuutazama ulimwengu huu tulio nao na uangalie uozo wa
wanadamu katika kujiheshimu, kisha ujiulize hivi kuna mwanaume au
mwanamke ambaye anaishi bila kumsaliti mpenzi wake? Baada ya swali hilo wachukue rafiki zako unaokunywa nao pombe na kufanya kazi nao kazi uone kama hamjawahi kuoneshana nyumba ndogo, baadaye fumba macho uiulize akili yako kuna asiyesalitiwa?
Wakati
unasubiri majibu endelea kuweka viashiria kichwani mwako kwa kumfikiria
mkeo anayemhudumia bosi chai huko ofisini au Muuguzi anayefanya kazi
chumba kimoja na Daktari usiku au askari polisi aliyeolewa anayekesha
lindoni na bachela, kisha subiri majibu kutoka kwenye ubongo wako!
Bila shaka kwa
mchakato huo mfupi tu majibu ya haraka yatakayokuja ni hakuna
asiyesalitiwa. Isipokuwa kuna kuuficha ukweli. Sasa kwa majibu hayo ya
akili mkeo unampenda nini wakati unafahamu kuwa anatoa penzi kwa wanaume
wenginekama wewe.
Thamani ya ndoa na umuhimu wako unatoka wapi, tuseme hupati uchungu pale unapohisi unaibiwa mumeo? Kamaunapata inakuwaje pale akili inapokupa majibu kuwa mkeo si mwaminifu?
Hapa ndipo
penye kiini cha somo letu kwamba, kuna wakati tunaruhusu mawazo yetu
yakimbie mwendo kasi kwenye njia yenye mabonde na kona na wengi wetu
tumeharibu ndoa zetu na wengine tumeachana na wapenzi wetu kwa ujinga wa
kutokuzuia kasi ya akili zetu.
Inashangaza kusikia na kuona kuna baadhi ya wanandoa wanaishi kwa kupelelezana kila siku kama askari
wakaguzi wa dawa za kulevya. Mke akichelewa kurudi lazima akaguliwe
kwanza kama hakutoka kupasha mwili nje, kadhalika mwanaume apimwe kwa
kunuswa kama hakuchepukia nyumba ndogo.
Hivi
tulishawahi kujiuliza kuwa tunautumia ubongo wetu vibaya kutafuta
ufumbuzi wa mambo ya kipuuzi!? Tunawafuatilia wake zetu maofisini kwao
ili iweje? Hatuaminiani kwa nini wakati tumeoana, je mapenzi yana faida
gani ndani ya usaliti na kujua kuwa sio wewe peke yako unayefaidi tunda
la mkeo au mumeo.
Wakati nikitafakari kuhusu mada hii kaka mmoja aliniambia kuwa amempata mchumba ambaye ni mzuri sana ,
anampenda na kumheshimu, lakini alitaka kujua atawezaje kumwamini kuwa
hatamsaliti? Kabla sijamjibu akajaza hoja nyingine kwamba kuna watu
kibao wanamsumbua mchumba wake kwa maana hiyo ana shaka kuna siku
atalegeza msimamo na kumsaliti!
Binafsi sikufikiria sana kumjibu
swali lake, bali nilimwambia kuwa jibu la swali lako ni KUJIMILIKISHA
UJINGA. Nikiwa na maana ile ile ya kudhibiti mwendo wa akili yake kwa
kuacha kuwaza mambo ambayo yanaashiria kutumia mwendo kasi wa akili
kwenye njia mbaya. Siku zote kushinda maisha kunahitaji uwezo wa
mwanadamu wa kujua ni wapi awaze sana na kupata ufumbuzi na wapi awaze kidogo au asiwaze.
Maana haiwezi
kuwa busara kwa mtu aliyemfuma mkewe na mwanaume mwingine atumie akili
kujua ilikuwaje mpaka kukawepo makubaliano au msukumo upi ulimvuta
mkewe kuutoa utu wake kwa mwanaume mwingine?
Inapofikia hatua hiyo umuhimu wa kulegeza mwendo wa akili kwa kusema sijui na sina haja ya kujua ilikuwaje, hata kamaakili
bado ina uwezo wa kujua mengine zaidi sema sitawaza juu ya jambo hili
la kipuuzi! Ukifanya hivyo utakuwa sawa na dereva anayeendesha gari
lenye injini yenye kasi kubwa lakini ameamua kwa makusudi tu kupunguza
mwendo kwa usalama wa maisha yake.
Hii ndiyo siri
ya usalama wa ndoa na uhusiano wa mapenzi ndani ya hofu ya usaliti.
Ukiona mawazo yanakuja kutaka kutoa jibu la kuchelewa kwa mumeo kurudi
huku dondoo za kuwepo kwa msichana mwingine kazini kwake zikichipuka,
yatupilie mbali mawazo hayo. NDOA MAANA YAKE NI KUAMINIANA. UKIONDOA
UAMINIFU HAKUNA NDOA!
0 comments:
Post a Comment