ads

Habari Mpya

Saturday, November 16, 2013

UCHAFU HUU KWENYE MITANDAO HAUSAIDII JAMII.

HAKUNA ubishi kwamba maisha ya binadamu yamerahisishwa sana kutokana na maendeleo ya tekinolojia hasa mapinduzi makubwa ya mawasiliano ya kompyuta. Maendeleo haya yamerahisisha ufanyaji kazi, yamepunguza mzigo wa uwasilishaji na kufikia taarifa mbalimbali.



Wakati zamani ilikuwa ni miujiza kujua nini kinatokea upande mmoja wa dunia kwa wakati mmoja, leo hii hali imerahisishwa mno, kila kitu kinachotokea kokote katika kona yoyote ya dunia kinaonekana na kufuatiliwa na kona nyingine kwa wakati huo huo.





Katika maendeleo haya, mawasiliano ya kompyuta ambayo kwa sasa yamesukumwa kwa nguvu kubwa zaidi na simu za mikononi ambazo nazo zinafanya kazi kama kompyuta, yamefanya kizazi cha sasa kufikia mafanikio makubwa sana ya kisayansi na kiuchumi kwa kasi kubwa.


Mataifa mengi yanatoa fursa za kuwekeza katika maendeleo ya mawasiliano na kompyuta kwa sababu ni dhahiri taifa ambalo litabaki nyuma katika nyanja hizo halitaweza kuhimili ushindani katika harakati za kujenga uchumi wake.


Tanzania kwa kipindi cha miaka zaidi ya 15 sasa imejibidiisha sana kutengeneza mazingira ya uwekezaji katika eneo hilo; mawasiliano ya njia ya kompyuta na simu za mkononi yameleta mapinduzi makubwa siyo ya kuzungumza tu, bali ya kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.


Wakati zamani ilikuwa ni ndoto wakazi wa vijijini kufikia taasisi za fedha kama benki, wakilazimika kusafiri umbali mrefu na kwa gharama kubwa kupata huduma za kibenki, siku hizi simu za mkononi zimegeuka kuwa benki; kadhalika wakati ilikuwa suala la kubahatisha kumtafuta mtu kwa kufunga safari hadi ufike eneo fulani, siku hizi ufungaji wa safari kama hizo umerahisishwa kwa kuwa na uhakika kwamba unayemfuata utamkuta na siyo tena jambo la kubahatisha, uhakika huu umeletwa na uhakika wa mawasiliano kokote aliko mtu kwa wakati wote kupitia simu za mkononi.


Maendeleo haya ya tekinolojia ya mawasiliano na kompyuta yanafurahiwa na kila mmoja, yanatumika kufanikisha mambo mengi makubwa kuanzia shughuli za uzalishaji mali, usafirishaji, upataji wa taarifa sahihi za masoko, utoaji elimu rasmi katika vyuo na shule, kushirikisha jamii katika maamuzi ya kuendesha mambo yao, kutaja kwa uchache tu.
 
 
Pamoja na faida hizi na nyingi ambazo hatuwezi kuziorodhesha hapa, wapo watu wabaya ambao badala ya kujikita kutumia vizuri tekinolojia hizi, wao wameamua kuingiza mambo ya kishenzi kabisa katika mawasiliano haya.


Wapo ambao wameamua kujiingiza katika uhalifu wa kutumia mitandao, hawa wanaiba fedha kwenye taasisi za fedha, kuingia katika akaunti za watu wengine na kukwapua fedha, na hata kughushi nyaraka na kufanikisha uhalifu wao.


Hawa wote wamesababisha tekinolojia hizi kuogopwa na baadhi ya watu kwa kuwa hawana uhakika sana juu ya usalama ama wa fedha zao au hata taarifa wanazofikia au kupelekewa.


Mbali na kundi hili la wahalifu wanaojinufaisha kwa kuiba, wapo wengine wanaotumia mwanya wa tekinolojia hii kuchafua wengine kwa kutengeza mambo ya kutunga.


Hii imepata kutokea mara nyingi hapa nchini. Washenzi hawa walipata hata kumchafua kiongozi mkuu wa nchi. Vyombo vya usalama vilifuatilia, lakini hadi leo umma haukupata fursa ya kujua au kuelezwa kama wahalifu hao walipatikana au la.


Wakati suala hilo likiwa limesahaulika, hivi karibuni mbunge mmoja naye amechafuliwa vivyo hivyo kwa picha zake kutengenezwa katika hali ya kumdhalilisha mno na kusambazwa kwa nguvu ya mitandao ya simu na kompyuta. Nia hasa ya ushenzi huo siyo kuwasiliana ila kuchafuana.


Tunasema kuwa katika dunia ya leo watakaofaidika na kusonga mbele katika mstari wa maendeleo ni jamii inayochangamkia fursa zinazopatikana kwa kutumia nyenzo ya mawasiliano ya simu za mkononi na kompyuta kufikia taarifa mbalimbali, kupata elimu, kushiriki katika kuboresha uzalishaji mali kwa faida yao na mataifa yao.


Hapa kwetu, wajuzi wa kutumia kompyuta badala ya kutumia fursa hiyo kwanza kujikwamua wenyewe kutoka kwenye lindi la umasikini, na pia kusaidia wengine, wao wanatumia nyenzo hizo kutengeneza picha chafu na kuzisambaza kana kwamba wanafanikisha jambo lolote la maana kwao na kwa taifa lao mbali tu ya kuzidi kuua jamii kimaadili.

 
Tunaamini vyombo vya ulinzi na usalama kwa miaka ya hivi karibuni vimejikita katika kujifunza jinsi ya kukabili uhalifu wa kimitandao (cyber-crime); mambo kama haya ya kutengeneza picha chafu na kuzisambaza yanaangukia moja kwa moja kwenye uhalifu huo.



Ni matumaini yetu kwamba sasa vyombo hivi vitatambua kuwa vina wajibu wa kupanua wigo wa kukabili uhalifu ikiwa ni pamoja na kwenye mitandao kama inavyoonekana kuwa unazidi kuongezeka mwaka baada ya mwaka.





Daima tukumbuke nia ya wagunduzi wa tekinolojia hizi ni kuongeza ufanisi na maendeleo ya binadamu, asilani siyo kuendeleza ushenzi wa kutunga matusi na uvunjaji wa maadili katika jamii. Tukatae ushetani huu unaotaka kufanywa sehemu ya maisha ya Watanzania. CHANZO: NIPASHE
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 comments:

Item Reviewed: UCHAFU HUU KWENYE MITANDAO HAUSAIDII JAMII. Description: Rating: 5 Reviewed By: Unknown
Scroll to Top